Romans 6

Kufa Na Kufufuka Pamoja Na Al-Masihi

1 aTuseme nini basi? Je, tuendelee kutenda dhambi ili neema ipate kuongezeka? 2 bLa hasha! Sisi tulioifia dhambi, tutawezaje kuendelea kuishi tena katika dhambi? 3 cAu hamjui ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Al-Masihi Isa tulibatizwa katika mauti yake? 4 dKwa hiyo tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti, ili kama vile Al-Masihi alivyofufuliwa kutoka kwa wafu kwa utukufu wa Baba, vivyo hivyo sisi nasi pia tupate kuenenda katika upya wa uzima.

5 eKwa maana ikiwa tumeungana naye katika mauti yake, bila shaka tutaungana naye katika ufufuo wake. 6 fKwa maana twajua kwamba utu wetu wa kale ulisulubiwa pamoja naye ili ule mwili wa dhambi upate kuangamizwa, nasi tusiendelee kuwa tena watumwa wa dhambi. 7 gKwa maana mtu yeyote aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi.

8 hBasi ikiwa tulikufa pamoja na Al-Masihi, tunaamini kwamba pia tutaishi pamoja naye. 9 iKwa maana tunajua kwamba Al-Masihi, kwa sababu alifufuliwa kutoka kwa wafu, hawezi kufa tena; mauti haina tena mamlaka juu yake. 10 jKifo alichokufa, aliifia dhambi mara moja tu, lakini uzima alio nao anamwishia Mungu.

11 kVivyo hivyo, jihesabuni wafu katika dhambi lakini mlio hai kwa Mungu katika Al-Masihi Isa. 12 lKwa hiyo, msiruhusu dhambi itawale ndani ya miili yenu, ipatikanayo na kufa, ili kuwafanya mzitii tamaa mbaya. 13 m nWala msivitoe viungo vya miili yenu vitumike kama vyombo vya uovu vya kutenda dhambi, bali jitoeni kwa Mungu, kama watu waliotolewa kutoka mautini kuingia uzimani. Nanyi vitoeni viungo vya miili yenu kwake kama vyombo vya haki. 14 oKwa maana dhambi haitakuwa na mamlaka juu yenu, kwa sababu hampo chini ya sheria, bali chini ya neema.

Watumwa Wa Haki

15 pNi nini basi? Je, tutende dhambi kwa kuwa hatuko chini ya sheria bali chini ya neema? La, hasha! 16 qJe, hamjui kwamba mnapojitoa kwa mtu yeyote kama watumwa watiifu, ninyi ni watumwa wa yule mnayemtii, aidha watumwa wa dhambi, ambayo matokeo yake ni mauti, au watumwa wa utii ambao matokeo yake ni haki? 17 rLakini Mungu ashukuriwe kwa kuwa ninyi ambao kwanza mlikuwa watumwa wa dhambi, mmekuwa watii kutoka moyoni kwa mafundisho mliyopewa. 18 sNanyi, mkiisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mmekuwa watumwa wa haki.

19 tNinasema kwa namna ya kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wenu wa hali ya asili. Kama vile mlivyokuwa mkivitoa viungo vya miili yenu kama watumwa wa mambo machafu na uovu uliokuwa ukiongezeka zaidi, hivyo sasa vitoeni viungo vyenu kama watumwa wa haki inayowaelekeza mpate kutakaswa. 20 uMlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa hamtawaliwi na haki. 21 vLakini mlipata faida gani kwa mambo hayo ambayo sasa mnayaonea aibu? Mwisho wa mambo hayo ni mauti. 22 wLakini sasa kwa kuwa mmewekwa huru mbali na dhambi na mmekuwa watumwa wa Mungu, faida mnayopata ni utakatifu, ambao mwisho wake ni uzima wa milele. 23 xKwa maana mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Al-Masihi Isa Bwana wetu.
Copyright information for SwhKC